Leviticus 22

Matumizi Ya Sadaka Takatifu

1 Bwana akamwambia Musa, 2 a“Mwambie Haruni na wanawe kushughulikia kwa uangalifu sadaka takatifu Waisraeli wanazoziweka wakfu kwangu, ili wasilinajisi Jina langu takatifu. Mimi ndimi Bwana.

3 b“Waambie: ‘Katika vizazi vijavyo, ikiwa yeyote wa wazao wako ni najisi kwa taratibu za kiibada, naye akakaribia sadaka takatifu zile Waisraeli wanazoweka wakfu kwa Bwana, mtu huyo lazima akatiliwe mbali na uso wangu. Mimi ndimi Bwana.

4 c“ ‘Ikiwa mzao wa Haruni ana ugonjwa wa ngozi unaoambukiza au anatokwa na usaha mwilini, hawezi kula sadaka takatifu mpaka atakasike. Pia atakuwa najisi ikiwa atagusa kitu chochote kilicho najisi kwa kugusa maiti au mtu aliyetokwa na shahawa, 5 dau ikiwa atagusa kitu chochote kitambaacho kimfanyacho mtu najisi, au mtu yeyote awezaye kumtia unajisi, hata unajisi uwe gani. 6 eMtu anayegusa kitu chochote cha aina hiyo atakuwa najisi mpaka jioni. Kamwe hatakula sadaka yoyote takatifu mpaka yeye mwenyewe awe ameoga kwa maji. 7 fWakati jua linapotua, atakuwa safi, na baadaye anaweza kula sadaka takatifu, kwa kuwa ni vyakula vyake. 8 gKamwe asile nyama ya mzoga wala iliyoraruliwa na wanyama pori, naye akatiwa unajisi kwa hilo. Mimi ndimi Bwana.

9 h“ ‘Makuhani lazima washike maagizo yangu ili wasiwe na hatia, wakafa kwa kuyadharau. Mimi ndimi Bwana ninayewafanya watakatifu.

10 i“ ‘Hakuna mtu yeyote asiye wa jamaa ya kuhani anayeruhusiwa kula sadaka takatifu, hata mgeni wa kuhani au mfanyakazi wake haruhusiwi kuila. 11 jLakini ikiwa kuhani amenunua mtumwa kwa fedha, au mtumwa amezaliwa katika nyumba ya kuhani huyo, mtumwa huyo aweza kula chakula cha huyo kuhani. 12Ikiwa binti wa kuhani ameolewa na mtu asiye kuhani, binti huyo haruhusiwi kula chochote cha matoleo matakatifu. 13Lakini ikiwa binti wa kuhani amekuwa mjane au amepewa talaka, naye hana watoto, na akarudi kuishi na jamaa ya baba yake kama wakati wa usichana wake, binti huyo anaweza kula chakula cha baba yake. Hata hivyo, mtu asiyeruhusiwa hawezi kula chochote katika chakula hiki.

14 k“ ‘Ikiwa mtu yeyote amekula sadaka takatifu kwa makosa, lazima atoe malipo ya sadaka hiyo kwa kuhani na kuongeza sehemu ya tano ya thamani ya sadaka hiyo. 15 lKamwe makuhani wasiinajisi sadaka takatifu ambayo Waisraeli wameitoa kwa Bwana 16 mkwa kuwaruhusu kuzila sadaka hizo takatifu, na hivyo kuwaletea hatia ya kudaiwa malipo. Mimi ndimi Bwana niwafanyaye watakatifu.’ ”

Dhabihu Zisizokubalika

17Bwana akamwambia Musa, 18 n“Sema na Haruni na wanawe, na Waisraeli wote uwaambie: ‘Ikiwa mmoja wenu, aliye Mwisraeli au mgeni anayeishi katika nchi ya Israeli, atatoa matoleo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Bwana, iwe kutimiza nadhiri au kuwa sadaka ya hiari, 19 olazima mtoe mnyama dume asiye na dosari, akiwa ng’ombe, mbuzi au kondoo, ili aweze kukubalika kwa niaba yako. 20 pKamwe usitoe kitu chochote chenye dosari kwa sababu hakitakubaliwa kwa niaba yako. 21 qMtu yeyote aletapo sadaka ya amani kwa Bwana kutoka kundi la ng’ombe au mbuzi ili kutimiza nadhiri maalum au sadaka ya hiari, lazima sadaka hiyo isiwe na dosari au waa ili ikubalike. 22Kamwe usimtolee Bwana mnyama aliye kipofu, aliyejeruhiwa wala aliye kilema, au chochote kilicho na uvimbe, au chenye upele au vidonda vinavyotoka usaha. Kamwe chochote cha aina hii kisiwekwe juu ya madhabahu kuwa sadaka iliyotolewa kwa Bwana ya kuteketezwa kwa moto. 23 rLakini waweza ukatoa ng’ombe au kondoo mwenye kilema au aliyedumaa kama sadaka ya hiari, lakini hii haitakubalika kuwa sadaka ya kutimiza nadhiri. 24 sKamwe usimtolee Bwana mnyama ambaye mapumbu yake yamejeruhiwa, au kuhasiwa, au kuraruliwa au kukatwa. Kamwe usifanye hivi katika nchi yako mwenyewe, 25 tna kamwe usikubali wanyama wa aina hii kutoka mkono wa mgeni ili kuwatoa wanyama hao kuwa chakula kwa Mungu wako. Wanyama hao hawatakubaliwa kwa niaba yako, kwa sababu wana vilema, nao wana dosari.’ ”

26Bwana akamwambia Musa, 27 u“Wakati ndama, mwana-kondoo au mwana-mbuzi azaliwapo, atabaki na mama yake kwa siku saba. Kuanzia siku ya nane na kuendelea anaweza kukubaliwa kuwa sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa kuteketezwa kwa moto. 28 vUsimchinje ng’ombe na ndama wake, au kondoo na kitoto chake siku moja.

29 w“Unapomtolea Bwana dhabihu ya shukrani, itoe kwa namna ambayo itakubalika kwa niaba yako. 30 xNi lazima iliwe siku iyo hiyo, pasipo kubakiza chochote mpaka asubuhi. Mimi ndimi Bwana.

31 y“Shikeni maagizo yangu na kuyafuata. Mimi ndimi Bwana. 32 zMsilinajisi Jina langu takatifu. Lazima nikubalike kuwa mtakatifu kwa Waisraeli. Mimi ndimi Bwana ninayewafanya watakatifu, 33 aana niliyewatoa katika nchi ya Misri niwe Mungu wenu. Mimi ndimi Bwana.”
Copyright information for SwhKC